Mahakama ya Homabay imeamuru kufanyiwa uchunguzi wa kiakili mwanamke anayedaiwa kumkata kichwa mwanawe katika kijiji cha Ng’ope kata ndogo ya Konyago kwa madai ya kukataa kunyonya.

Hakimu Mkuu wa mahakama hiyo Mary Ochieng’ ameagiza mshukiwa Night Akoth Otieno kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Homabay ili kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kubaini iwapo ana akili timamu.

Hakimu Ochieng ameagiza mshukiwa kurejeshwa mahakamani Jumatatu wiki ijayo ili kusomewa mashtaka ya mauaji.

Wakaazi wanasema mshukiwa ambaye anaripotiwa kutokuwa na akili timamu alichukua panga na kumkata mwanawe Briton Ochieng’ ambaye alikuwa analia baada ya kukataa kunyonya.

Wakaazi waliojawa na ghadhabu walimfunga mshukiwa mikono na miguu wakitaka kumuua lakini akaokolewa na naibu Chifu wa eneo hilo aliyempeleka katika kituo cha polisi.