Rais Uhuru Kenyatta amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Marekani Joe Biden.

Kuu kwenye mazungumzo hayo ya kina imekuwa ni namna ya kuboresha uhusiano wa karibu baina ya Kenya na Marekani.

Kimsingi, rais Kenyatta na Biden wameshauriana kuhusu kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo mawili, uchumi, amani, usalama, mabadiliko ya tabia nchi, haki za kibinadamu pamoja na mgogoro katika upembe wa Afrika.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena amearifu kuwa rais Biden alizingatia umuhimu wa Kenya na Marekani kuendelea kushirikiana na hakikisho kwamba taifa lake litasalia kuwa mshirika wa karibu wa Nairobi.

Kuhusu usalama, rais Biden amesisitiza kwamba Marekani itaendelea kujitolea kushirikiana na Kenya kuleta amani na usalama katika kanda hii ikiwemo katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Biden alipongeza Kenya kwa kuwa katika mstari wa mbele kupigana na ugaidi, kuinua uchumi sawa na kutafuta suluhu la kudumu katika mzozo wa Tigray, Ethopia na kukomesha mauaji zaidi.