Chama cha ODM kimeongeza muda kwa wanaotaka kutuma maombi ya kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 kwa tiketi ya chama hicho.

Katika taarifa, mwenyekiti wa bodi ya kitaifa ya uchaguzi katika chama hicho Catherine Mumma amesema muda huo umeongezwa kutoka hapo kesho Februari 26 hadi Machi 31 mwaka huu.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho tayari ametuma maombi ya kupata tiketi ya chama hicho kuwania urais huku akielezea matumaini kwamba atawashinda wenzake watakaotuma maombi.

Kwa mujibu wa chama hicho, anayetaka kuteuliwa ni sharti awe raia wa Kenya kwa kuzaliwa, awe mpiga kura aliyesajiliwa, awe mwanachama wa maisha wa ODM na awe na digrii kutoka chuo kikuu kinachotambulika.

Aidha, ni lazima walipe ada ya Shilingi Milioni moja pesa ambazo hawatarudishiwa.