Wabunge wako huru kuanza kujadili mswada wa marekebisho ya katiba BBI baada ya kupokea dhibitisho kutoka kwa mabunge 30 ya kaunti yaliyopitisha mswada huo.
Spika wa bunge la kitaifa Justine Muturi na mwenzake wa bunge la Senate wamedhibitisha kupokea maamuzi kutoka kwa mabunge hayo ikiwemo Nairobi kama inavyohitajika kisheria.
Mabunge hayo ni pamoja na Siaya, Homa Bay, Kisumu, Trans Nzoia, Busia, Kajiado, Pokot Magharibi, Laikipia, Kisii, Nairobi, Garissa, Mombasa, Nyamira, Taita Taveta, Kakamega, Kitui, Vihiga, Murang’a, Narok, Makueni, Kirinyaga, Nyeri, Bungoma, Machakos, Nakuru, Meru, Bungoma, Tharaka Nithi, Embu, Marsabit, Nyandarua, Kericho na Tana River.
Hata hivyo Muturi amesema bunge la kaunti ya Baringo ambalo ni la kipekee kukataa mswada huo kufikia sasa lilikosa kuwasilisha mswada uliokataliwa na hivyo kufanya vigumu kujua ni nini walichokikataa.
Kufuatia hatua hiyo, bunge la kitaifa na lile la Seneti wanatazamiwa kuanza kushughulikia mswada huo bila kuchelewa kwani tayari kanuni zote zimezingatiwa.