Kesi ya ufisadi inayomkabili Gavana wa Kaunti ya Migori Okoth Obado na washukiwa wengine sasa itasikilizwa katika Mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi.

Hii ni baada ya Jaji James Wakiaga kutupilia mbali ombi la mmoja wa watuhumiwa wenza wa gavana ambaye alitaka kesi hiyo ihamishwe na kusikizwa katika mahakama ya Migori.

Wakiaga amebaini kuwa ombi hilo lilitolewa na mtu mmoja tu, maanake washukiwa wengine wanaoshtakiwa wameridhishwa na kesi yao kusikilizwa katika mahakama ya Nairobi.

Gavana Obado na wenzake ambao si wa familia yake wanakabiliwa na kesi ya ufisadi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji kuwashtaki kwa kosa la kuiba Sh73 millioni pesa za Kaunti ya Migori.