Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala zake za rambirambi kwa rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kufuatia kifo cha makamu wa rais wa kwanza Maalim Seif Sheriff, (77).

Rais Kenyatta kwenye ujumbe wake amemtaja Maalim Seif kama mwanasiasa mwenye hekima na ambaye mchango wake kwa aliowaongoza na katika kanda ya Afrika kwa jumla utakumbukwa.

Wakati uo huo, rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza siku 3 za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha Maalim Seif Sharif Hamad.

Maombolezo hayo yataanza leo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni, rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi amesema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.

Maalim Seif amefariki dunia akiwa ametumikia wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais wa SMZ kwa chini ya siku 100 – akiwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020.

Kifo chake kinahitimisha safari ya kisiasa ya mwanasiasa mashuhuri kuliko wote wa Zanzibar na kiongozi ambaye alizibeba siasa za upinzani katika visiwa hivyo katika muda wa miaka 30 iliyopita.