Bunge la kitaifa limebuni kamati maalum kuongoza mipango ya mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Bonchari John Oroo Oyioka aliyefariki usiku wa kuamkia leo.

Spika wa bunge hilo Justine Muturi ametangaza kuwa kamati hiyo itaongozwa na mbunge wa Borabu Ben Momanyi.

Wanachama wengine kwenye kamati hiyo ya mazishi ni wabunge Richard Onyonka (Kitutu Chache), Samwel Arama (Nakuru Mjini), Joash Nyamoko (North Mugirango), Richard Tongi (Nyaribari Chache), Jerusha Momanyi (Nyamira) miongoni mwa wengine.

Yakijiri hayo

Wabunge wametumia vikao vya alasiri ya leo kuwaomboleza aliyekuwa seneta Yusuf Hajji na aliyekuwa mbunge Oroo Oyioka.

Wabunge wakiongozwa na Spika Justine Muturi wamewataja wenda zao kama viongozi waliojitolea kulihudumia Wakenya kwa weledi.

Oyioka alifariki katika hospitali ya Aga Khan kaunti ya Kisumu ambapo alikuwa anapokea matibabu.

Marahemu alihifadhi kiti chake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 kupitia kwa chama cha Peoples Democratic PDP kabla ya kuteuliwa mwanachama wa kamati ya elimu, utafiti na teknolojia.