Mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyekiri kumchapa na kumuumiza mwalimu wake amehukumiwa kifungo cha nje cha miezi kumi na nane huku mahakama ikiagiza ahamishwe hadi shule nyingine.

Samwel Muigai Migwi amepewa hukumu hiyo na hakimu mkaazi wa mahakama ya Nyahururu James Wanyanga.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Januari 18, 2021 katika shule ya upili ya Murichu, Muigai alimtandika na kumsababishia majereha mwalimu wake aliyekuwa kwenye zamu kwa ngumi na mateke baada yake kumuuliza ni kwa nini alikuwa anaruka laini wakati wa mlo.

Katika kujitetea kwake, mwanafunzi huyo aliiomba mahakama imsamehe na akahaidi kuwa raia mwema mwenye kufuata sheria.

Aidha aliahidi kumuomba mwalimu wake msamaha na kudhibiti hasira zake.

Muigai anatarajiwa tena mahakamani Disemba 16, 2021 wakati ripoti kuhusu mienendo yake itaangaziwa.