Ushawahi kuskia kisa cha marehemu kumuibia marehemu? Amini usiamini ndicho kisa ambacho kimewakosesha usingizi maafisa wa idara ya upelelezi nchini DCI hadi walipowakamata washukiwa watano hapo jana.

Washukiwa hao walitumia nambari ya simu ya marehemu Kasisi Peter Kariuki, aliyekuwa katibu mkuu wa kanisa la PCEA, kuiba pesa kutoka kwa akaunti za benki za mfanyibiashara marehemu Amos Ngata Muiruri.

Watano hao ambao watafikishwa mahakamani hii leo wanamiinika kuwa miongoni mwa genge ambalo linabadilisha kadi za simu za marehemu pindi anapofariki kabla ya kumuibia pesa alizokuwa nazo kwa simu na pia benki na kisha, kutumia nambari yake pia kuibia watu wengine.

Genge hilo limekuwa likitumia magazeti ya kila siku nchini kufahamu haswa matajiri wanaofariki na kutumia muda wa maombolezo kwa familia kuibia wapendwa wao ambao wamefariki.

Katika taarifa, idara ya upelelezi nchini DCI inasema washukiwa wanatumia muda wa maombolezo kwani ndio wakati familia haiwezi kushuku kuna wizi unaendelea.

Katika kisa  cha hivi karibuni, washukiwa hao walitumia nambari ya marehemu kasisi Kariuki kuiba zaidi ya shilingi million mbili nukta nane kutoka kwa akaunti za benki za mfanyibiashara huyo marehemu Njeru, wote hao ambao walifariki na kuzikwa mwezi Julai na Disemba mtawalia mwaka uliopita.

Familia ya mfanyibiashara huyo ilishuku kuna ukora ulikuwa unaendelea baada ya simu ya marehemu kuacha kufanya kazi mara moja.

Familia ya kasisi Kariuki kwa upande wao, haikuwa na ufahamu kuwa nambari ya simu ya mpendwa wao waliyemzika inatumika kuwaibia watu wengine.

DCI inasema wengine wanaolengwa kwenye wizi huo ni wakongwe na pia watu wanaosafiri kwenda ughaibuni, na haswa matajiri.

Washukiwa watafunguliwa mashtaka hii leo katika mahakama ya Milimani.