Kaunti za Pokot Magharibi na Busia zimekuwa za hivi punde kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Kaunti ya Busia imekuwa ya nne huku Pokot Magharibi ikiwa ya tano kupitisha mswada huo katika vikao vilivyoandaliwa hii leo.

Katika bunge la kaunti ya Busia, idadi kubwa ya madiwani walipitisha mswada huo huku mmoja pekee akipinga.

Spika wa bunge hilo Benard Wamalwa amesema atawafahamisha rasmi spika wa bunge la kitaifa na mwenzake wa Senate kuhusu uamuzi huo.

Katika bunge la kaunti ya Pokot Magharibi, hali ilikuwa ni iyo hiyo spika Catherine Mukenyang akisema mswada huo ulipitishwa na bunge hilo kwa kauli moja.

Kaunti ya Pokot Magharibi inayoongozwa na gavana John Lonyangapuo imekuwa ya kwanza katika eneo la bonde la ufaa kupitisha mswada huo uliokataliwa na kaunti ya Baringo ambayo ndio ya kwanza kufanya hivyo.

Mswada huo unapendekeza, miongoni mwa masuala mengine, kuongezwa kwa mgao wa pesa kwa serikali za kaunti na pia MCAs kutengewa hazina yao ya maendeleo.

Pokot Magharibi na Busia sasa zinajiunga na kaunti za Homabay, Kisumu na Siaya ambazo zimepitisha mswada huo huku kaunti ya Baringo ikiutupilia mbali.

Mswada huu wa BBI unahitaji kupitishwa na angalau kaunti 24 kati ya 47 ili kura ya maamuzi kufanyika.