Seneta wa Garissa Yusuf Haji amefariki mapema hii leo akipokea matibabu katika kaunti ya Nairobi.
Familia yake ilidhibitisha kuwa Haji alifariki katika hospitali ya Agha Khan, Nairobi akipokea matibabu.
Haji alisafirishwa hadi nchini Turkey mwishoni mwa mwaka uliopita kwa matibabu kabla ya kurejeshwa nchini siku ya Jumamosi na kulazwa tena katika hospitali ya Agha Khan amabapo amefariki akipokea matibabu.
Haji alikuwa waziri wa usalama wa ndani kutoka mwaka wa 2008-2013 kwa serikali ya rais mstaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.
Aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuongoza jopo la BBI ambalo lilitoa ripoti inayopendekeza mabadiliko kadhaa katika katiba.
Haji ambaye alizaliwa Disemba mwaka wa 1940 ni babake mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Noordin Haji.
Alichaguliwa mwaka 2013 kuwa seneta wa Garissa na kuingia bungeni ambapo amehudumu katika kamati mbalimbali ikiwemo ile ya usalama.
Rais Uhuru Kenyatta amewaongoza wakenya kumuomboleza Haji.
Katika rambirambi zake, Rais amemtaja Haji kama kiongozi wa kutegemewa na mzalendo huku akitaja kifo chake kama pigo kwa taifa
Kenyatta amesema Kenya itakosa uongozi wa Haji haswa katika mchakato wa BBI na kuiombea familia yake faraja.
Kwa upande wake Naibu rais William Ruto amesema Haji alikuwa mwanasiasa mwenye hekima na alikuwa kiongozi bora
Kinara wa ODM Raila Odinga amesema anamshukuru Haji kwa kazi ambayo alifanya akiwa hai na bidii aliyotia kupigia debe BBI
Bunge la Kitaifa limesema Haji alikuwa kiongozi wa kipekee aliyeongoza taifa kwa moyo mmoja.
Haji atakumbukwa katika mchango wake kuandaa ripoti ya BBI kufuatia mwaka baina ya Rais Kenyatta na Odinga.
Marahemu atazikwa hii leo saa kumi katika makaburi ya Langata kaunti ya Nairobi.
Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiangi amedokeza kuwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto watahudhuria ibada ya kumuaga mwendazake ambayo inafanyika mtaai South C baadaeye hii leo.