Idadi ya maambukizi ya corona nchini imefikia 102,048 baada ya watu 104 kupatikana na virusi hivyo kati ya sampuli 3,348 kupimwa katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita.

Katika taarifa waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema watu 69 wamepona na kufikisha idadi ya waliopona kuwa 84,542.

Wagonjwa 3 zaidi wameaga na kufikisha idadi ya maafa nchini kuwa 1,789.

Watu 368 wamelazwa katika hospitali mbalimbali wengine 1,315 wanashughulikiwa nyumbani.

Idadi ya wagonjwa walio katika hali mahututi ni 37.

Msambao katika kaunti ni kama ifuatvyo Nairobi 68, Laikipia 7, Kiambu 6, Uasin Gishu 6, Siaya 3.

Yakijiri hayo

Inspekta mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai amewataka maafisa wa Polisi kuhakikisha kuwa masharti ya kuzuia msambao wa virusi vya corona yametekelezwa kikamilifu.

Mutyambai katika taarifa amesema umma umelegeza masharti hayo ya usalama licha ya taifa kuendelea kuripoti visa vichache vya ugonjwa wa corona.

Miongoni mwa masharti ambayo Mutyambai anasema yamepuuzwa ni pamoja na kuandaliwa kwa mikutano ya kisiasa pasipo kuzingatia masharti ya usalama na baadhi ya wafanyibiashara kupuuza muda wa kafyuu ambao ni saa nne usiku.

Inspekta wa Polisi vile vile amesema baadhi ya magari ya uchukuzi wa umma yanabeba abiria kupitia kiasi wengi wao wakikosa kuvalia barakoa.

Mutyambai katika taarifa hiyo ameonya kuwa watakaopuuza masharti hayo watachukuliwa hatua za kisheria.