Utoaji wa kati za Huduma Namba umeanza rasmi katika kaunti ya Nairobi.

Wizara ya usalama wa ndani inasema Wakenya wataenda kuchukua kadi hizo pindi watakapopata ujumbe mfupi.

Katika taarifa, wizara hiyo imesema kadi hizo tayari zimefikishwa katika vituo mbalimbali vya Huduma tayari kuchukuliwa na wenyewe.

Serikali imeashiria kwamba inapania kuondoa vitambulisho vya kitaifa na nafasi hiyo kuchukuliwa na kadi za Huduma kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Rais Uhuru Kenyatta na mkewe Margaret Kenyatta walikuwa wa kwanza kupata kadi hizo Octoba 20 mwaka jana wakati wa sherehe za Mashujaa katika uwanja wa Gusii mjini Kisii.