Chama cha ODM kitamuunga mkono muwaniaji wa chama cha Wiper Agnes Kavindu kwenye uchaguzi mdogo wa useneta utakaoandaliwa Machi 18.

ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kimesema kitamuunga mkono Kavindu kwa sababu ya ushirikiano wa muungano wa NASA na mchakato wa BBI.

Haya yanajiri siku moja baada ya mwenyekiti wa ODM tawi la Machakos Peter Matuku kutangaza kuwa chama hicho kingemuunga mkono Mutua Katuku wa chama cha Maendeleo Chap Chap.

Kavindu alipigwa jeki kwenye azma yake ya kuwa seneta wa Machakos baada ya viongozi Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Moses Wetangula wa FORD-K na Gideon Moi wa KANU kumpigia debe wikendi iliyopita.

Mbali na wawaniaji wengine, Kavindu anatazamiwa kupambana na Urbanus Ngengele wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Katuku wa Maendeleo Chap Chap.