Wawaniaji wa viti vya ubunge vya Matungu na Kabuchai kaunti za Kakamega na Bungoma mtawalio wameanza kampeini za kuomba kura saa chache baada ya kuidhinishwa na tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya aliye pia naibu kiongozi wa chama cha ODM amewaongoza wabunge akiwemo kiranja wao bungeni Junet Mohamed kumpigia debe muwaniaji wa kiti hicho katika eneo la Matungu David Were ambaye ni mbunge wa zamani.

Nao wabunge ambao ni wendani wa naibu rais William Ruto wakiongozwa na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa wamempigia debe muwaniaji wa kiti cha ubunge katika eneo la Kabuchai kwa tiketi ya chama cha UDA Alex Lanya.

Chaguzi hizo za Matungu na Kabuchai zinatarajiwa kuandaliwa Machi 4 kufuatia vifo vya Justus Murunga na James Lusweti.