Kwa siku ya pili mfululizo Kenya imeandikisha idadi kubwa ya wagonjwa waliokufa kutokana na corona.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe anasema watu 26 wamefariki kutokana na ugonjwa huo katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita na kufikisha idadi ya maafa kuwa 1,180.

Mhudumu mmoja zaidi wa afya amefariki kutokana na ugonjwa huo na kufikisha idadi ya wahudumu wa afya waliofariki kuwa 23 huku walioambukizwa wakiwa 2,148, wakiwemo wanaume 1,087 na wanawake 1,061.

Maambukizi ya virusi hivyo yanazidi kupanda huku watu 1,216 wakikutwa na virusi hivyo baada ya kupima sampuli 6,816 na hivyo kufikisha idadi ya visa hivyo nchini kuwa 65,804.

Idadi ya waliopona ugonjwa huo imeongezeka na kufikia 43,626 baada ya kupona kwa watu 531 huku waliolazwa hospitalini wakiwa 1,289, 51 wako katika chumba cha watu mahututi ICU.