Katibu mkuu wa muungano wa walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri (KUPPET) tawi la Uasin Gishu Elijah Maiyo amemtaka waziri wa elimu Profesa George Magoha kuomba msamaha kufuatia matamshi yake alipozuru shule ya msingi ya Langas wiki jana.

Maiyo anasema licha ya kwamba Profesa Magoha alipata shule hiyo ikiwa na uchafu huku mjengo ukiendelea, halikuwa jambo la ustaarabu kwake kuwaagiza walimu na wanafunzi kuokota taka hata kama alikuwa amekasirishwa.

Katibu huyo wa KUPPET amesema itawalazimu kutumia sheria kumshurutisha Magoha iwapo hataomba radhi kwani hawatakubali mtu wa hadhi yake kutumia lugha ya matusi dhidi ya wadogo wake.

Kwenye video inayosambaa mitandaoni, waziri Magoha anasikika akimuabisha na hata kumtukana mkurugenzi wa elimu katika kaunti hiyo Gitonga Mbaka kwa kuzembea kazini.