Wanafunzi 68 na walimu 5 wa shule ya upili ya wasichana Bahati kaunti ya Nakuru wamepatikana na virusi vya Corona na kupelekwa karantini.

Akidhibitisha taarifa hiyo, waziri wa afya katika kaunti hiyo Daktari Kariuki Gichuki amesema wanafunzi wengine 115 wamewekwa karantini na wanaendelea kushughulikia.

Mwanafunzi mmoja ameonekana kulemewa na virusi hivyo na amekimbizwa hadi katika hospitali ya rufaa ya Nakuru anapokea matibabu.

Gichuki amesema kundi la madaktari limekuwa likipeana mafunzo kuhusu ugonjwa huo katika shule mbalimbali yanayolenga walimu, wanafunzi na wafanyikazi wa shule.

Gichuki amewasihi wakaazi wa Nakuru kuendelea kufuata maagizo kutoka kwa wizara ya afya kujikinga na ugonjwa wa Corona.