Rais Uhuru Kenyatta ametangaza kukaza kamba kwenye masharti ya kudhibiti msambao wa virusi vya corona baada ya kuongezeka kwa idadi ya virusi hivyo.

Akitangaza masharti hayo baada ya kukutana na baraza la magavana, rais amesema mwezi wa Octoba ulishuhudia taifa hili likiandakisha visa 15,000 vya ugonjwa huo huku watu 300 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuongeza kafyuu ya kutotoka nje kati ya saa nne usiku na saa kumi asubuhi na itaendelea hadi Januari 3, 2021.

Shule zitasalia kufungwa hadi Januari mwaka ujao ila wanafunzi wa darasa la nne, darasa la nane na kidato cha nne wataendelea na masomo yao chini ya uangalizi wa hali ya juu ili kuwalinda dhidi ya maambukizi.

Mawaziri vile vile wametakiwa kupunguza shughuli za kuonana ana kwa ana huku watumishi wa umma walio na umri wa miaka 58 wakitakiwa kufanya kazi wakiwa nyumbani.

Shughuli za maabadi hazitaathirika ila masharti yaliyokuwepo yatasalia kuzingatiwa.

Mikahawa pamoja na maeneo ya burudani imetakiwa kufungwa kufikia saa tatu usiku.