Familia moja huko Kathiani, kaunti ya Machakos inalilia haki baada ya mwanao mwenye umri wa miaka 11 kudhulumiwa kimapenzi na washukiwa wawili ambao ni babu na mjomba wa mwanao.

Msichana huyo mwanafunzi wa darasa la tano anasema wawili hao wamekuwa wakimdhulumu kimapenzi tangu mwaka 2016 kabla ya mamake kugundua kuwa mwanawe hayuko sawa.

Akisumulia namna babuye alimshawishi kushiriki naye tendo hilo pasipo kuzingatia umri wake, msichana huyo ambaye tunabana majina yake kwa sababu za kiusalama anasema mzee huyo alianza kwa kumdanganya kuwa angempa vitamu iwapo angekubali kulala naye.

Anasimulia kuwa mjombake naye alianza kumtendea kitendo hicho tangu mwaka 2016 huku akimtishia maisha iwapo angedhubutu kumwambia yeyote.

Licha ya kwamba imemchukua muda mrefu kugundua, kwa machungu, mamake mtoto huyo anaeleza alibaini kilichokuwa kinaendelea baada ya kumpata mwanawe akilia huku machozi yakimtiririka.

Katika kile kinachoonekana kama kutilia msumari moto kwenye kidonda, mumewe ambaye ni babake mtoto huyo amemfukuza nyumbani kisa na maana anapigania haki ya mwanao.