Waziri wa afya Mutahi Kagwe na mwenzake wa Uchukuzi James Macharia wanatazamiwa kuhojiwa na bunge hii leo kuhusu madai ya kupotea kwa vifaa vya kupambana na janga la corona kutoka kwa wakfu wa Jack Ma.
Kagwe na Macharia wanatazamiwa kufika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya kuelezea ukweli kuhusu vifaa hivyo na namna pesa zilizotengwa kupambana na janga hilo zilivyotumika.
Wawili hao watajibu maswali ya wabunge kuhusu ni vipi barakoa zaidi ya alfu mia moja pamoja na vifaa vya kupima corona vilipotea kwa njia zisizoeleweka punde tu baada ya kuwasili nchini mnamo mwezi Machi.
Waziri Kagwe ambaye ametajwa kwenye sakata ya kupotea kwa pesa katika shirika la dawa KEMSA anatazamiwa kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu madai hayo na namna pesa za COVID19 zimetumika.