Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wamemuomboleza mkurugenzi mkuu wa chama cha Jubilee James Waweru aliyefariki leo akipokea matibabu katika hospitali ya Karen, kaunti ya Nairobi.

Rais Kenyatta kwenye rambirambi zake amesema taifa hili limempoteza kiongozi mchapa kazi aliyejitolea kulihudumia kwa bidii kwa miaka nyingi.

Rais amesema marehemu ambaye wakati mmoja alihudumu kama katibu mkuu katika Wizara ya Michezo na mkuu wa wilaya wakati wa uongozi wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki aliacha nyayo za kufuatwa katika idara aliyohudumia.

Naye naibu rais William Ruto kwa upande wake ameifariji familia ya Waweru akisema taifa limempoteza kiongozi aliyefanya kazi kwa kujitolea.

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga vile vile ametuma risala zake za rambirambi kufuatia kifo hicho.