Wapiga kura Machakos wanaelekea debeni Alhamisi hii kumchagua seneta wao huku tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) ikisema kila kitu kiko shwari.

IEBC imetakiwa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wazi.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ambaye anamuunga mkono muwaniaji wa chama cha Wiper Agnes Kavindu ameitaka IEBC kuhakikisha kuwa imezima visa vyote vya wapiga kura kuhongwa na ghasia.

Kwa mujibu wa IEBC, Machakos ina wapiga kura 622,965 waliosajiliwa, maeneo bunge 8, wadi 40 na vituo vya kupigia kura 1,335.

Kinyanganyiro kimewavutia wawaniaji 11 akiwemo Agnes Kavindu wa chama cha Wiper, Urbanus Ngengele wa United Democratic Alliance (UDA), John Musingi wa chama cha Muungano miongoni mwa wengine.

Muwaniaji wa chama cha Maendeleo Chap Chap Mutua Katuku alijiondoa kwenye kinyanganyiro hicho

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa seneta Boniface Kabaka mwezi Disemba mwaka uliopita.