Afisi kuu za kaunti ya Kirinyaga zimefungwa kwa muda wa wiki mbili zijazo kuanzia hii leo kutokana na kuongezeka kwa virusi vya corona.

Akitoa tangazo hilo Gavana Anne Waiguru amesema baadhi ya maafisa wa serikali yake wamefariki kutokana na virusi hivyo huku wengine kadhaa wakiambukizwa.

Waiguru amesema maafisa hao watakuwa wanafanya kazi kutoka nyumbani huku akiagiza wizara ya afya katika kaunti yake kuwapima maafisa kutoka idara zote zilizoathirika na kutoa majibu ya vipimo haraka.

Hata hivyo Gavana huyo ametoa hakikisho kwa wakaazi wa Kirinyaga kuwa idara zote muhimu zitaendelea kufanya kazi na kwamba wameweka mikakati ya kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya corona.