Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amempongeza rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kushinda uchaguzi wa urais ulioandaliwa Oktoba 28.

Rais Kenyatta amesema kuchaguliwa kwa Magufuli kuongoza kwa muhula wa pili kunaashiria matumaini walio nayo Watanzania katika uongozi wake.

Katika ujumbe wake wa kumhongera, rais Kenyatta amemtakia Magufuli afya njema anapoanza kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa awamu nyingine huku akimuhakikishia kuwa Kenya itaendelea kushirikiana naye kwa manufaa ya rais wake.

Haya yanajiri huku upinzani ukiitisha maandamano kuanzia Jumatatu Novemba 2 kupinga matokeo ya uchaguzi huo kwa misingi kwamba ulikumbwa na udanganyifu.

Viongozi wa upinzani wakiongozwa na Tundu Lissu wa chama cha CHADEMA na Freeman Mbowe wameitisha maandamano ya amani kushinikiza kufanyika upya kwa uchaguzi mwingine.

Tume ya uchaguzi nchini humo NEC ilimtangaza Magufuli wa chama tawala cha CCM kama rais mteule kwa kupata kura 12,516,252 ambayo ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa.

Tundu Lissu aliibuka wa pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote ziizopigwa.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki licha ya pingamizi za upinzani.