Waliokuwa vigogo wa muungano wa upinzani NASA wameunga mkono ripoti ya maridhiano BBI walipohudhuria hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Vigogo hao Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper na Moses Wetangula wa chama cha FORD K kwa kauli moja hata hivyo wametoa wito wa kurekebishwa kwa maswala wanayoyohisi kwamba yanahitaji kuangaziwa upya ikiwemo ugatuzi na hali ya uchumi.

Na katika kile kinachoonekana kama mwanzo mpya, wazazi wa mtoto wa miezi sita Samantha Pendo aliyeuawa wakati wa vurugu za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 wamezungumza kwa umma baada ya kumpoteza mwanao.

Lencer Achieng na Joseph Abanja waliokuwepo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya maridhiano BBI katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi wamewatadharisha wanasisasa dhidi ya kusababisha uhasama wa kisiasa wakati wa uchaguzi na kusababisha maafa ya watu wasiokuwa na hatia.

Baby Pendo aliuawa baada ya kupigwa risasi na maafisa wa Polisi nyumbani kwao Nyalenda, Kisumu wakati wa kupambana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.