Viongozi wa kidini wanataka kuharakishwa kwa mchakato wa kujaza nafasi za makamishna wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) waliojiuzulu.

Viongozi hao chini ya muungano Dialogue Reference Group wanasema inatia wasiwasi kuona kwamba bunge limepuuza jukumu lake la kuanzisha mchakato wa kujaza nafasi hizo ilhali uchaguzi mkuu wa 2022 unakaribia.

Wanapendekeza kubuniwa kwa kamati ya pamoja ya bunge kuanzisha mchakato huo wa kuwatafuta makamishna wapya pasipo kuwa na mwingilio wa kisiasa.

IEBC aidha imetakiwa kuwapa Wakenya taarifa za mara kwa mara kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo wa 2022 badala kuwaacha gizani.

Haya yanajiri siku moja baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwapendekeza waliokuwa makamishna watatu wa IEBC Margaret Mwanchanya, Consolata Nkatha na Paul Kurgat kuwa mabalozi.