Ili kuhakikisha kuwa Wakenya wanakuwa na imani na matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022, rais Uhuru Kenyatta ameshauriwa kuhakikisha kuwa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imebuniwa kikamilifu.

Wito huu umetolewa na gavana wa Machakos Dkt. Alfred Mutua ambaye anasema kubuniwa kwa tume hiyo mapema kutaipa muda wa kutosha kujiandaa vilivyo kwa uchaguzi huo.

Akizungumza alipopeleka kampeini zake za kuwania urais katika kaunti ya Laikipia, kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap amesema kubuniwa kwa tume hiyo kunafaa kuambatana na mapendekezo yaliyotolewa na iliyokuwa tume ya Kriegler iliyopendekeza kubuniwa kwa tume ya uchaguzi miezi kumi na minane kabla ya uchaguzi.

Hayo yakijiri

Viongozi wa kidini wanataka kuharakishwa kwa mchakato wa kujaza nafasi za makamishna wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) waliojiuzulu.

Haya yanajiri siku moja baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwapendekeza waliokuwa makamishna watatu wa IEBC Margaret Mwanchanya, Consolata Nkatha na Paul Kurgat kuwa mabalozi.

Viongozi hao chini ya muungano Dialogue Reference Group wanasema inatia wasiwasi kuona kwamba bunge limepuuza jukumu lake la kuanzisha mchakato wa kujaza nafasi hizo ilhali uchaguzi mkuu wa 2022 unakaribia.

Wanapendekeza kubuniwa kwa kamati ya pamoja ya bunge kuanzisha mchakato huo wa kuwatafuta makamishna wapya pasipo kuwa na mwingilio wa kisiasa.

IEBC aidha imetakiwa kuwapa Wakenya taarifa za mara kwa mara kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo wa 2022 badala kuwaacha gizani.

Haya yanajiri siku moja baada ya rais Uhuru Kenyatta kuwapendekeza waliokuwa makamishna watatu wa IEBC Margaret Mwanchanya, Consolata Nkatha na Paul Kurgat kuwa mabalozi.