Chama cha mawakili nchini (LSK) kimewasilisha kesi mahakamani kupinga masharti mapya yaliyotolewa na kamati ya usalama kutuliza joto la kisiasa nchini.

LSK kwenye kesi yake inaiomba mahakama kubatilisha agizo linalowataka Polisi kuwapa kibali wanaonuia kuandaa mikutano kwa misingi kwamba ni ukiukaji wa katiba.

Chama hicho kinahoji kwamba utekelezwaji wa masharti hayo utahujumu haki na uhuru sawa na ilivyo kwenye katiba.

Walioshtakiwa kwenye kesi hiyo ni Inspekta mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai na mwanasheria mkuu Kihara Kariuki.

Hayo yanajiri huku Mutyambai akitetea idara hiyo kuhusina na shtuma kuwa wanaegemea upande mmoja katika kutekeleza sheria za kudhibiti mikusanyiko.

Akijibu maswali kutoka kwa Wakenya kupitia kwa ukurasa wa Twitter, Mutyambai amesema wamekuwa wakiruhusu mikutano kutoka kwa baadhi ya makundi ambayo hayajakuwa na vurugu na kuzuia mikutano ya wanasiasa ambao mikutano yao imekuwa ikikumbwa na vurugu.

Mutyambai amesema kibali cha kuandaa mikutano kinategegemea na iwapo kuna athari ya kukumbwa kwa vurugu au la.

Anasema hawatasita kuendelea kufutilia mbali mikutano ambayo kuna uwezekano wa kuzuka kwa ghasia.