Mshukiwa wa uhalifu kutoka mtaani Sauti ya Engine eneobunge la Kapseret kaunti ya Uasin Gishu amejitoa uhai ili asikamatwe baada ya kufumaniwa na maafisa wa polisi.

Katika taraifa, idara ya upelelezi nchini DCI inasema mshukiwa ambaye alifumaniwa baada ya kuiba pikipiki kwa ushirikiano na washukiwa wengine watatu, alitumia kisu cha jikoni kujikata koo alipofahamu kuwa njama yao imefahamika.

Washukiwa hao walikuwa wameiba pikipiki kutoka kwa jamaa mmoja jana usiku eneo la Berur na kumuacha akiwa amezirai lakini alipopata fahamu, alipigia polisi simu ambao walianza msako.

Washukiwa watatu, Zedrick Mulama, Robert Safari na Silas Lugalia walikamatwa na pikipiki hiyo ya wizi huku pia pikipiki zingine tatu zinazoaminika kuwa za wizi zikipatikana katika maficho yao.

Watatu hao waliwaelekeza polisi alikokuwa mashukiwa wa nne ambaye alipofahamu njama yao imetibuka, alichukua kisu na kujtoa uhai ili asikamatwe.