Baadhi ya wabunge waasi wa Chama Jubilee wamehudhuria mkutano wa wabunge wa Muungano wa Kenya Kwanza iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi hii leo. 

Wabunge hao waliongatuliwa chamani katika Mkutano wa Wajumbe wa Kitaifa wa Chama hicho (N.D.C) ulioandaliwa siku ya jana tayari wametangaza kuunga mkono utawala wa  Rais William Ruto.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo uliongozwa na Rais Ruto ni pamoja na Mbunge wa EALA Kanini Kega anayeongoza uasi dhidi ya Kinara wa chama cha Jubilee Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni akidai kuwa wawili hao sio viongozi halali.

‘’Aliyekuwa Rais (Kenyatta)  ameamua kukaidi agizo la Kamati ya nidhamu ya chama cha jubilee.  Yeye sio kiongozi wa chama chetu. Hana uwezo wa kuita au kusimamia mkutano wowote wa chama. Ameibisha afisi ya Rais Mstaafu.’’ Alisema Kioni.

Wanachama wengine wa Jubilee waliohudhuria mkutano ikuluni ni  Pamoja na Mbunge Mteule Sabina Chege aliyetangazwa kuwa kinara mpya wa chama hicho na kundi la waasi, Adan Keynan (Eldas), Fatma Dullo (Seneta Isiolo) na Yusuf Hassan (Kamukunji) .

Miongoni mwa ajenda muhimu zilizojadiliwa  ikuluni hii leo ni pamoja na  mswaada wa bajeti 2023/2024  ambao umeibua hisia mseto  miongoni mwa wakenya wengi wakikashifu pendekezo la nyongeza ya ushuru unaotozwa kwa bidhaaa mbalimbali na mikato ya mishahara.

Katika hotuba yake katika NDC iliyoandaliwa jana Rais Kenyatta alisema kuwa amelazimika kurejea kwenye siasa kutokana na malumbano chamani.

“Nilitaka kuondoka katika ulingo wa kisiasa na nilikuwa nikifikiria katika NDC ndipo ningejitokeza kutangaza kustaafu kwangu,” aliwaambia wajumbe katika uwanja wa michezo wa Ngong jijini Nairobi.

Akionekana kumshambulia mrithi wake, Rais William Ruto, Kenyatta aliapa kukabiliana na waaasi wa chama Jubilee.

“Baadhi ya watu wameamua kuwa kazi yao itakuwa ya dhuluma na kutishia wengine. Leo nakuambia utafute mtu mwingine sio Uhuru Kenyatta,” alisema Kenyatta.