Wendani wa naibu rais William Ruto wamejitokeza kumtetea saa chache baada ya rais Uhuru Kenyatta kumtaka adhubutu kujiuzulu iwapo amechoka.
Maseneta Kichumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet na Susan Kihika wa Nakuru badala yake wamemuambia Ruto akae ngumu.
Kihika kwenye ukurasa wake wa Twitter amemuambia Ruto kwamba ‘’wapiga kura zaidi ya milioni saba waliompatia kazi Octoba mwaka 2017 bado hawajachoka naye na kumtaka kukaa ngumu’’.
Murkomen naye kwa kutumia ukurasa uo huo wa Twitter amesema ‘’sio mtu fulani pekee anafaa kujiuzulu kwa sababu hata yule mwingine yuko huru kufanya hivyo kikatiba’’.
Uhuru akihojiwa na wahariri amesema jambo muhimu kwa Ruto kufanya kwa sasa ni kuondoka serikalini badala ya kuendelea kuikosoa ilhali yuko ndani.