Afisa wa Polisi wa kituo cha Njoro, Nakuru amemuua kwa kumpiga risasi mpenziwe aliyekuwa anatibiwa na kisha akajitoa uhai kwa kujipiga risasi.

Ripoti ya Polisi inaonesha kuwa mwendo wa saa saba usiku, Mary Nyambura, 29 alifika katika hospitali ya Njoro akiwa na jeraha la mguu akisema alikuwa ameumizwa na mpenziwe.

Madaktari wakiendelea kumshughulikia, Polisi Benard Sivo, 28 aliyekuwa amejihami aliingia katika hospitali hiyo na kumpiga risasi mara kadhaa mwanamke huyo na kumuua papo hapo.

Baadaye polisi huyo aliyekuwa ameingia kwenye zamu alianza kufyatua risasi kuholela na kuhatarisha maisha ya wenzake.

Juhudi za kumnyanganya bunduki yake aina ya AK 47 ziliambulia patupu kwani alijigeukia na kujipiga risasi lililongilia kwenye kidevu na kutokea kichwani na kufariki papo hapo.