Chama cha Jubilee sasa kiko tayari kuingia kwenye muungano na chama cha ODM baada ya viongozi wake wakuu kuidhinisha pendekezo hilo.

Katika taarifa, katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amesema viongozi wakuu wa chama hicho sawia na viongozi wao bungeni wamekutana leo na kuafikiana kwa kauli moja kubuni muungano na ODM.

Tuju anasema wanalenga pia kushirikisha chama cha KANU, Wiper, Amani National Congress na Ford Kenya kwa muungano huo wa kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti tisa hapo mwakani.

Kamati kuu ya chama hicho imesema uamuzi huo umetokana na ushirikiano mwema baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, uhusiano ambao anasema umeshabikiwa na jamii ya kimataifa.

Hatua hii ina maana kuwa ODM na Jubilee watakuwa na mgombea mmoja wa Urais kwenye uchaguzi hao.

Tayari Rais Kenyatta amenukuliwa akisema Odinga ndiye anafaa zaidi kumrithi.