Wafanyikazi kadhaa wa serikali eneo bunge la Bahati kaunti ya Nakuru wamesimamishwa kazi baada ya watu kumi kufariki kwa kubugia pombe haramu.

Mshirikishi wa bonde la ufa George Natembeya anasema miongoni mwa waliosimamishwa kazi ni naibu kamishna Godfrey Mwami, Kamanda Bernard Wamuginda, OCS Solomon Wamae, D.O Isaac Ooko, chifu na manaibu wake wawili, miongoni mwa wengine.

Natembeya amesema wanalenga kumaliza uuzaji wa pombe haramu kwa muda wa wiki moja ijayo na kutoa onyo kwa maafisa wa serikali wanaozembea kazini ilhali wananchi wanaumia.

Kumi hao walifariki baada ya kubugia pombe inayoaminika kuwa kemikali kali aina ya methanol.