Maafisa wa polisi waliohusika katika kukamatwa kwa ndugu wawili waliofariki eneo la Kianjokoma huko Embu wamesimamishwa kazi.

Inspekta mkuu Hilary Mutyambai anasema faili ya uchunguzi wa mauaji hayo tayari imekabidhiwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ambaye atapendekeza mashtaka watakayofunguliwa.

Mutyambai amekariri kuwa haki itatendeka kwa ndugu hao Benson na Emmanuel Ndwiga waliofariki mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa kwa kuwa nje wakati wa kafyu.

Inspekta huyo ametoa wito kwa umma kutoa nafasi kwa asasi za usalama kumaliza mchakato wa kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa marahemu.