Naibu rais William Ruto sasa anasema amelazimika kuliomba taifa la Uturuki msamaha kwa niaba ya serikali ya Kenya baada ya raia wake Harun Aydin kufurushwa nchini.

Ruto kupitia kwa mtandao wa Twitter amedai kuwa Harun alikamatwa kwa sababu za kisiasa, kuteswa, kuwekelewa madai ya ugaidi na kisha kufukuzwa.

Naibu rais amelalamikia siasa kuingizwa katika maswala yenye umuhimu wa kitaifa na yana uwezo wa kuharibu uchumi wa taifa hili.

Wakili wa raia huyo Ahmednasir Abdullahi anadai kuwa hakufurushwa ila aliagizwa kuondoka nchini Kenya kwa hiari.

Hata hivyo Ahmednassir anasema hawajui sababu zipi zilifanya kuondolewa nchini kwa mteja wake kwani walitarajia afikishwe mahakamani leo.

Wakili huyo akiwa ameandamana na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi amedai kuwa serikali imekiuka sheria za kimataifa kwa kumfurusha nchini raia huyo bila kumfikisha mahakamani na kumpa nafasi ya kujitetea.

Aydin alikamatwa siku ya Ijumaa wakati alirejea humu nchini kutoka Ethiopia katika safari ambayo alifaa kuandamana na Dr Ruto.

Yakijiri hayo, Ruto amewataka wapinzani wake wa kisiasa kukoma kupuuzilia mbali mfumo wake wa kiuchumi na badala yake watafute mfumo wao.

Akizungumza baada ya mkutano wa siku mbili ambapo alikutana na viongozi kutoka eneo la Nyanza kunadi sera zake, Ruto ameelezea kuridhishwa kwake na namna mjadala wa kisiasa ulivyobadilika nchini.