Bunge la kaunti ya Nyamira limeidhinisha uteuzi wa Dr James Gesami Ondicho kuwa naibu Gavana wa kaunti hiyo.

Gesami sasa ataapishwa kuwa naibu wa pili wa gavana baada ya Amos Nyaribo kuapishwa kuwa Gavana kufuatia kifo cha aliyekuwa Gavana John Nyagarama.

Waakilishi wadi wa Nyamira wamekubaliana kwa kauli moja kuidhinisha uteuzi wa Gesami licha ya kamati ya uteuzi kukataa kuidhinisha uteuzi wake awali kwa madai ya kutokuwa na cheti cha maadili na pia idhini kutoka kwa chama chake.

Gesami amewahi kuhudumu kama mbunge wa Mugirango Magharibi kwa mihula miwili.

Baadhi ya wafuasi wa Gesami waliokuwa nje ya bunge hilo walishangilia kwa nyimbo pindi waliposkia taarifa za kuidhinishwa kwa Gesami.