Huku wanafunzi wakiendelea kujiunga na kidato cha kwanza, serikali imetoa Sh17.4b kufadhili masomo katika shule za msingi na za upili.
Shule za msingi zitapata Sh2.6b huku shule za sekondari zikitazamiwa kupata mgao mkubwa wa Sh14.8b.
Kufuatia hatua hiyo, waziri wa elimu Prof. George Magoha amewataka wakuu wa shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanasalia shuleni kuendelea na masomo ikizingatiwa kwamba kalenda ya masomo ni fupi mno.
Waziri Magoha vile vile amewaonya wakuu wa shule dhidi ya kuitisha pesa zingine kutoka kwa wazazi na kuwataka kuzingatia mwongozo wa karo uliotolewa.
Profesa Magoha pia ametaka wazazi kuhakikisha kwamba wanafunzi wamejiunga na kidato cha kwanza zoezi hilo likiendelea kote nchini.