Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ameshtakiwa kwa kumuumiza mwanakandarasi Stephen Masinde aliyekuwa akidai pesa zake alizotumia kukarabati madarasa ya shule moja katika eneobunge hilo.

Barasa amekanusha mashtaka dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja na mdhamini wa kiasi sawia na hicho huku kesi hiyo ikiratibiwa kuanza kuskilizwa tarehe 27 mwezi ujao wa tisa.

Licha ya kukana mahakamani, Barasa amekiri nje ya mahakama kuwa alimzaba kofi mwanakandarasi huyo na kujitetea kuwa alikuwa amemchokoza.

Kizaazaa kiliibuka katika shule ya msingi ya Lurare wadi ya Kamukuywa siku ya Ijumaa wakati mwanakandarasi huyo alifunga madarasa yaliyokuwa yakizunduliwa kushinikiza alipwe pesa alizotumia kuyajenga.

Badala yake mbunge huyo alipandwa na hamaki na kumzaba kofi.