Polisi mtoro Caroline Kangogo aliuawa kupitia risasi moja la kichwa.

Matokeo ya upasuaji ulioendeshwa na mpasuaji mkuu wa serikali Dr. Johansen Oduor yanaonesha kwamba risasi hilo liliingia moja kwa moja hadi akilini mwake.

Bila kufichua mengi, Dr. Oduor amesema kulikuwa na shimo la risasi kichwani mwake.

Hata hivyo kitendawili cha iwapo au la Kagongo alijipiga risasi hakijateguliwa huku uchunguzi zaidi wa mahabara ukitazamiwa kufanywa kubaini ukweli.

Upasuaji huo umefanyika katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Moi, Eldoret baada ya kuhamishwa kutoka hifadhi ya hospitali ya kaunti ndogo ya Iten.

Kangogo anadaiwa kujipiga risasi ndani ya bafu ya nje nyumbani kwa wazazi wake Anin, kaunti ya Elgeyo Marakwet na kufikisha kikomo msako dhidi yake kwa madai ya kuua wanaume wawili akiwemo polisi mwenzake John Ogweno.

Shughuli ya ukaguzi wa maiti iliratibiwa kufanyika Ijumaa wiki iliyopita lakini ikahairishwa hatua ambayo ilizua hamaki miongoni mwa familia iliyopanga kumzika Jumamosi iliyopita.