Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua atasalia rumande wikendi hii akisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu ijayo.

Mwanasiasa huyo alikamatwa Ijumaa asubuhi nyumbani kwake Sagana kaunti ya Nyeri na amepelekwa katika kituo cha Polisi cha Gigiri baada ya kuhojiwa katika makao makuu ya idara ya upelelezi DCI.

Wapelelezi wa DCI wanachunguza sakata ya Sh12b zinazohusishwa na akaunti za mbunge huyo.

Mbunge huyo amekaribisha hatua ya kukamatwa kwake akisema inampa nafasi ya kusafisha jina lake mahakamani kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Hata hivyo mbunge huyo anaendelea kusema kukamatwa kwake kumechochewa na mchango wake katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kiambaa.

Kumetokea maandamano kwenye barabara kuu ya Nyeri-Nairobi kupinga kukamatwa kwa mbunge huyo.

Iliwalazimu Polisi wa kupambana na ghasia kutumwa ili kuzima maandamano hayo yaliyotatiza usafiri kwenye barabara hiyo.