Tume ya uwiano na utangamano wa kitaifa (NCIC) imeongoza mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu na viongozi wa kaunti ya Marsabit kufuatia majuma kadhaa ya mapigano ya kikabila.

Mwenyekiti wa tume hiyo Kasisi Samwel Kobia amesema mazungumzo hayo yamefanyika kufuatia agizo la rais Uhuru Kenyatta baada ya kukutana na viongozi wa kaunti hiyo katika Ikulu ya rais jijini Nairobi.

Mkutano huo wa siku mbili uliowakutanisha gavana, seneta pamoja na wabunge umeafikia kwamba kila mmoja achukue jukumu la kibinafsi kuleta amani na mshikamano.

Viongozi hao wameunda mkakati wa pamoja watakaotumia kuhubiri amani na kuzileta jamii za kaunti hiyo pamoja.