Rais wa muda wa Mali Assimi Goita yuko salama baada ya kutibuka kwa jaribio la kumshambulia kwa kisu leo Jumanne.

Maafisa wa usalama wanasema rais huyo alishambuliwa akitoka katika maombi ya Eid al-Adha kwenye mji mkuu wa Bamako.

Mshukiwa aliyejaribu kumshambulia rais huyo kwa kisu alilemewa na walinzi wa Goita ambao walifaulu kumzuia kumfikia.

Afisa mmoja kutoka afisi ya rais ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Goita yuko salama huku shirika la habari la Reuters likiripoti kwamba limefahamishwa na wanajeshi kwamba rais huyo hakujeruhiwa.