Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ametoa wito kwa vitengo vya usalama kushirikiana na mahakama kumaliza dhulma, kupotea na pia mauaji ya kinyama ya watoto na akina mama.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Odinga amesema watoto wengi na akina mama wamepoteza maisha yao mikononi mwa watu ambao wanafaa kuwalinda bila hatua kuchukuliwa dhidi yao.

Odinga amesema visa hivyo havikubaliki kamwe na kuitaka idara ya usalama kuwahakikishia wakenya usalama wao na kuahidi kuwa hakuna mtoto au mwanamke atadhulumiwa au kuuwawa wakitazama

Waziri huyo mkuu wa zamani ametoa wito kwa mahakama pia kuharakisha kesi za washukiwa wa mauaji ili haki kutendeka kwani kucheleweshwa kwa uamuzi wa kesi hizo kunachangia ongezeko la dhuluma na mauaji.

Haya yanajiri baada ya mshukiwa mwingine sugu wa mauaji Evans Wanjala kukamatwa kwa madai ya kuua watoto watano katika eneo la Moi’s Bridge kaunti ya Uasin Gishu.