Mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita (ICC) imedhibitisha mashitaka dhidi ya wakili Mkenya Paul Gicheru.

Mahakama hiyo yenye makao yake nchini Uholanzi imesema kuna misingi ya kutosha kuhakiki kwamba Gicheru alihusika na njama ya kuhujumu mchakato wa kupatikana kwa haki.

Wikili Paul Gicheru anatuhumiwa kuhitilafiana na kesi dhidi ya naibu rais William Ruto na mwanahabari Joshua Arap Sang mnamo Septemba 10, 2015.

Mahakama hiyo imeeleza kuwa mashahidi 8 walifichua kwamba Gicheru na wenzake walikula njama ya kuwatambua na kisha kuwasiliana na mashahidi kwenye kesi hizo ambapo walijitolea kuwapa pesa au msaada mwingine ili kubatilisha ushahidi wao.

Gicheru alijisalimisha kwa mahakama hiyo Novemba 2, 2020 baada ya waranti ya kukamatwa kutolewa dhidi yake.