Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i amewapatia waliohusika na mauaji ya watu 11 huko Kerio Valley makataa ya siku 7 kujisalimisha.

Akitangaza makataa hayo baada ya kuongoza mkutano wa kiusalama katika kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi, waziri Matiang’i ameonya kuhusu uwezekano wa kuendeshwa kwa zoezi la kuwapokonya watu silaha haramu ili kukomesha visa vya utovu wa usalama.

Mkutano huo umeandaliwa katika kanisa la AIC la Tot kufuatia ongezeko la visa vya utovu wa usalama katika kaunti hizo.

Viongozi hao wamekubaliana kushirikiana na asasi za usalama kuleta amani na usalama.

Magavana Stanley Kiptis (Baringo), John Lonyangapuo (Pokot Magharibi) na Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) walihudhuria mkutano huo.