Aliyekuwa mbunge wa Gwasi Felix Nyauchi amekuwa na wakati mgumu kujibu maswali alipokuwa anahojiwa kwa wadhifa wa kuwa kamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.

Zaidi ya mara moja wakili huyo alikuwa na ugumu kujieleza wakati mwingine makamishna wa jopo hilo wakilazimika kusonga mbele na maswali mengine.

Jopo hilo linaloongozwa na Dr. Elizabeth Muli pia lilimhoji mtalaamu wa maswala ya uongozi Omore Osendo ambaye alijitetea kwa kusema kwamba una uzoefu wa kutosha kusimamia uchaguzi.

Dr. Dinah Jeruto kutoka kaunti ya Nakuru vile vile alipata fursa ya kuhojiwa huku akielezea ni kwa nini anapaswa kuteuliwa kuwa kamishna wa IEBC.

Watatu hao wanajiunga na wenzao watano ambao tayari wamehojiwa akiwemo mtafiti wa maswala ya sera Caroline Nganga, mfanyikazi wa IEBC Catherine Kamindo na wakili wa mahakama kuu Cecilia Ngoyoni.

Wengine ni wakili Anne Mwikali na Dr. Abdirazak Nunow waliohojiwa wa kwanza.