Mahojiano ya kuwatafuta makamishna wapya wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC) yameingia siku yake ya pili Alhamisi huku watu watatu wakihojiwa.
Mtafiti wa maswala ya sera Caroline Nganga amenadi sera zake mbele ya jopo linaloendesha mahojiano hayo chini ya uenyekiti wake Dr. Elizabeth Muli na kuahidi kusaidia tume hiyo kuzuia migogoro ya uchaguzi iwapo atateuliwa.
Jopo hilo vile vile limemhoji mfanyikazi wa IEBC Catherine Kamindo ambaye amewatetea wenzake kuhusiana na shutuma za kila mara huku akisema ana imani na uongozi wa mwenyekiti Wafula Chebukati.
Wakili wa mahakama kuu Cecilia Ngoyoni kutoka Marsabit amefunga ukurasa wa mahojiano hayo kwa siku ya pili akisema ana ufahamu wa kutosha kuhusu maswala ya uchaguzi.
Wengine waliohojiwa kwenye siku ya kwanza ni wakili Anne Mwikali na Dr. Abdirazak Nunow huku Abdalla Mohamed akijiondoa kwa kuwa na stakabadhi ghushi.