Mahojiano ya kuwatafuta makamishna wanne wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC yameng’oa nanga katika jumba la kimataifa la mikutano KICC.
Abdalla Mohamed aliyeratibiwa kuhojiwa wa kwanza amejiondoa baada ya kubainika kuwa alighushi stakabadhi zake za masomo.
Mwenyekiti wa jopo linaloendesha mahojiano hayo Elizabeth Muli amesema naibu chansela wa chuo kikuu cha Methodist amewaandikia waraka kuwajulisha kuwa Mohamed hakuwa mwanafunzi wa chuo hicho wala hawakumpa cheti cha digrii alivyodai.
Mohamed ambaye alituma waraka wa kujiondoa baada ya kuibuka kwa kisa hicho na Muli sasa anataka asasi husika kumchunguza.
Wakili Anne Mwikali alikuwa na wakati mgumu kujitetea huku swala tata la kuhairishwa kwa uchaguzi mkuu likiibuka.
Mwingine aliyehojiwa ni Dr. Abdirazak Arale Nunow aliyenadi sera zake mbele ya jopo hilo.
Jumla ya watu 36 watahojiwa hadi tarehe 22 mwezi huu kutafuta watakaojaza nafasi za makamishna waliojiuzulu; Roselyn Akombe, Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na Connie Maina.